2 Kings 9

Yehu Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme

1 aNabii Al-Yasa akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, uichukue hii chupa ya mafuta, na uende Ramoth-Gileadi. 2Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Enda kwake, umtenge na wenzake, na umpeleke katika chumba cha ndani. 3Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake, nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”

4Basi yule kijana nabii akaenda Ramoth-Gileadi. 5Wakati alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.”

Yehu akauliza, “Kwa yupi miongoni mwetu?”

Akamjibu, “Kwako wewe, jemadari.”

6 bYehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Bwana, yaani Israeli. 7 cInakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Bwana iliyomwagwa na Yezebeli. 8 dNyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru. 9 eNitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya. 10 fKuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.

11 gYehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?”

Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”

12Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.”

Yehu akasema, “Haya ndiyo aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”

13 hWakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”

Yehu Anamuua Yoramu Na Ahazia

14 iBasi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu, 15 jlakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.” 16 kNdipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.

17Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.”

Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

18Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”

19Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”

Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”

20 lYule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”

21 mYoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. 22 nYoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?”

Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”

23 oYoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”

24 pKisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake. 25 qYehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Bwana alipotoa unabii huu kumhusu: 26 r‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Bwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Bwana.”

27 sWakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko. 28 tWatumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi. 29 u(Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)

Yezebeli Auawa

30 vKisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake rangi, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani. 31 wYehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”

32Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama. 33Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo baadhi ya damu yake ikatapanyika ukutani na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.

34 xYehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti wa mfalme.” 35Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono. 36 yWakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Bwana alilosema kupitia kinywa cha mtumishi wake Ilya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataikula nyama ya Yezebeli. 37 zMaiti ya Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwepo mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ndiye Yezebeli.’ ”
Copyright information for SwhKC